quinta-feira, 9 de fevereiro de 2012

Nchi yatikisika

Nchi yatikisika

9th February 2012
Hospitali Kuu zote huduma hakuna
Wanaharakati wafunga barabara Dar
Hoja yazimwa mara sita Bungeni
Wanaharakati wakianadamana na mabango kwenye makutano ya barabara za Ocean na Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam jana kwa lengo la kushinikiza Serikali isikilize madai ya madaktari ili kumaliza mgomo wao unaoendelea nchini.(Picha: Khalfan Said)
Mgomo wa madaktari katika hospitali mbalimbali sasa umeitikisa nchi huku madaktari zaidi wakiungana na wenzao kuishinikiza serikali kusikiliza madai yao.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameamua kuacha vikao vya Bunge kwa ajili ya kusaka suluhu na madaktari.
Hayo yakiendelea, jana wanaharakati waliandamana na kufunga barabara jijini Dar es Salaam kwa saa moja kushinikiza serikali itatue mzozo wa madaktari ambao sasa unakaribia mwezi mmoja.
Mjini Dodoma nako, wabunge walicharuka ikiwa ni mara ya sita hoja ya kutaka kujadili mgomo wa madaktari inaibuka lakini ikizimwa, huku wanasiasa nje ya Bunge wakitoa matamko ya kuitaka serikali kuchukua hatua.
Pinda jana, alilazimika kuondoka bungeni na kurejea jijini Dar es Salaam kutafuta ufumbuzi wa mgomo huo ambao umesababisha vifo vya wagonjwa kuongezeka na wengine kuondolewa na ndugu zao katika hospitali za serikali.
Akizungumza na madaktari wa Hospitali ya Temeke jana, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, alisema Waziri Mkuu ameamua kuacha vikao vya Bunge ili kutafuta suluhu na madaktari waliogoma.
Alisema wakati Pinda anatafuta ufumbuzi wa mgomo huo, ni vema madaktari wa Hospitali hiyo waakarudi kazini kwa ajili ya kuokoa maisha ya wananachi.
“Kabla ya kuja hapa, nilikuwa uwanja wa ndege kumpokea Waziri Mkuu ambaye amekuja aghfla kwa ajili ya kutafuta suluhu ya jamabo hili, nawaomba madaktari rudini kazini wakati mnasubiri hatua zitakazochukuliwa,” alisema.
TEMEKE HALI MBAYA
Hali katika Hospsitali ya Temeke imezidi kuwa mbaya. Imeelezwa idadi ya watu wanaokufa imengezeka na kufikia watu 39 kwa siku kutoka 15 katika siku za kawaida.
Sadiki alisema baada ya Hospitali ya Muhimbili kusitisha huduma, tegemeo kubwa lilikuwa kwa Hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala, hivyo hatua ya kugoma hawatawatendea haki wananchi wasio na uwezo wa kwenda katika hospitali binafsi.
“Chonde chonde ndugu zangu, tuamue sasa kurudi kuwahudumia wananchi hawa, wengi ni maskini, nipo tayari kutatua baadhi ya kero kama mlivyoniambia,” alisema Sadiki.
Awali madaktari hao walimwambia Sadiki kuwa wameamua kugoma baada ya kuzidiwa na wagonjwa wanaotoka Muhimbili.
Dk. Ronald Mkonye alieleza kwamba udaktari upo ndani ya mioyo, lakini sio kitu kizuri Serikali kuwalazimisha, badala yake iangalie madai yao.
“Mkuu wa Mkoa hawa watu wanakabiliwa na matatizo mengi, hapa hakuna vifaa na pia tumezidiwa na wagonjwa wanaotoka Muhimbili, tulichoamua hapa si kugoma ila tumeshindwa kutokana na wingi wa watu,” alisema Dk. Mkonye.
Akizungumza na NIPASHE, mfanyakazi wa chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali hiyo, Mohamed Bakari, alisema kuanzia juzi vifo vya wagonjwa viliongezeka na kufikia 39 wanaokufa kwa siku wakati chumba hicho kina uwezo wa kuhifadhi maiti 15 kwa siku.
“Tumezidiwa mno baada ya kutokea mgomo, hatuna sehemu ya kuhifadhi maiti imetubidi tuziweke tatu tatu kwenye jokofu na zingine tumezilaza chini,” alisema Bakari.
Katika wodi namba mbili maalum kwa watoto, vitanda vilionekana kuwa tupu baada ya wagonjwa kuondolewa na ndugu na kuwapeleka kwenye hospitali binafsi na zahanati za jirani.
Mwanamke mmoja ambaye alionekana akiwa na mtoto wake mgongoni akijiandaa kuondoka, alisema ameamua kumnusuru mtoto wake kwa kumpeleka kwenye hospitali zingine angalau akapatiwe huduma. “Toka jana (juzi) hatukupatiwa matibabu, hali ya mtoto wangu ni mbaya, nimeamua kumchukua niende hospitali zingine,” alisema.
Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Amani Malila, alisema huduma iliyosimamishwa ni kwa wagonjwa wa nje, lakini wagonjwa wa dharura na watoto wataendelea kupatiwa matibabu.
OCEAN ROAD NAO WAGOMA
Madaktari wa Taasisi ya Saratani (Ocean Road), jana walijuunga na mgomo huo. Mgomo wa madaktari wanaotoa huduma ya mionzi na x-ray ulisababisha usumbufu kwa wagonjwa waliofika kupata huduma hiyo.
NIPASHE lilishuhudia msongamano mkubwa wa wagonjwa waliokuwa wanasubiri huduma hizo wakati uongozi wa hospitali hiyo ukiwasihi madaktari hao kuendelea na kazi.
Mwanahamisi Juma, mgonjwa aliyevunjika miguu kwa ajali ya gari aliyefika kupata huduma ya x-ray alisema: “Nimekuja hapa tangu asubuhi, lakini sijapata huduma yoyote, nimeambiwa madaktari wamegoma na sasa hivi wapo kwenye kikao.”
Jackson Richard, aliyefika Hospitalini hapo kupata huduma ya mionzi, alisema: “Nilipangiwa tarehe ya leo nije kupata huduma ya mionzi, lakini tangu nifike sijapata huduma, tumeambiwa madaktari wamegoma na wapo kwenye kikao.”
WAGONJWA WAHAMISHWA MUHIMBILI
Katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, hali ya utoaji huduma ilikuwa duni, hali iliyowalazimisha ndugu na jamaa kuwahamisha wagonjwa wao na kuwapeleka hospitali binafsi.
Sauda Kasimu, ambaye ndugu yake Aidali Mussa aliyelazwa Wodi ya Sewahaji alisema: “Nimeamua kumhamisha mgonjwa wangu kumpeleka TMJ kwa kuhofia hali yake kuwa mbaya zaidi.”
WAGONJWA BUGANDO WATESEKA
Mgomo wa madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza umesababisha mateso kwa wagonjwa.
NIPASHE ilipofika hospitalini hapo, lilishuhudia huduma zote za kitabibu zikiwa zimesimama, zikiwemo za upasuaji.
“Mimi ninaishangaa kwa kuthamini fedha, badala ya kusikiliza madai ya madaktari kiasi cha kusababisha usumbufu pamoja na vifo kwa wagonjwa kutokana na mgomo huu,” alilalamika mgonjwa mmoja ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Joseph Gilyoma, hakuwa tayari kuzungumza lolote kuhusiana na mgomo huo.


RUFANI MBEYA WABADILI MBINU
Madaktari katika Hospitali ya Rufani ya Mbeya, wamebadili mbinu ya mgomo na kutii amri ya Serikali ya kuwataka kurejea kazini, lakini hawatoi huduma kwa wagonjwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali hiyo, Dk. Humphrey Kiwelu, alisema jana kuwa madaktari waliokubali kurejea kazini wanafika na kusaini kitabu cha mahudhurio, lakini hawatoi huduma kwa wagonjwa.
Alisema kati ya madaktari 75 wa hospitali hiyo waliogoma, 10 kati yao ni waajiriwa wa Serikali na wengine 65 walikuwa ni madaktari walioko katika mafunzo kwa vitendo hospitalini hapo.
Alisema madaktari hao 10 waajiriwa wa Serikali, saba kati yao wamerejea kazini, lakini wanashirikiana na madaktari 65 walio katika mafunzoni ambao wanafika na kusaini kitabu cha mahudurio kisha kuondoka bila kutoa huduma kwa wagonjwa, hali ambayo inasababisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa kuendelea kuwa ngumu.
Kufuatia hali hiyo, Dk. Kiwelu alitoa wito kwa wananchi wanaohitaji huduma za afya waanzie katika vituo vya afya, hospitali za wilaya na ikishindikana hapo waende hospitali ya Mkoa na kwamba ikionekana mgonjwa anazidi kuwa na hali mbaya ndipo apelekwe katika Hospitali hiyo baada ya maagizo ya daktari wa Hospitali ya Mkoa.
KCMC SIO SHWARI
Utoaji huduma katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro bado si wa kuridhisha huku wauguzi wakitoa huduma kwa kushirikiana na madaktari wanafunzi kutoka katika chuo cha KCMC na vyuo vingine.
Madaktari waliogoma hadi jana walikuwa wakiripoti asubuhi kama kawaida na kuondoka na kuwaachia madaktari waliopo katika mafunzo kwa vitendo.
Gazeti hili lilishuhudia baadhi ya vitanda katika wodi ya wagonjwa wa mifupa na wale waliopata ajali pamoja na wodi ya wazazi na ya watoto vikiwa wazi kutokana na wagonjwa kuhamishwa na kupelekwa katika hospitali binafsi.
WABUNGE WAMTEMBELEA MUHIMBILI
Kamati ya Bunge za Huduma ya Jamii ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Margaret Sitta, ilitembelea Hospitali ya Muhimbili na kupita katika wodi kujionea hali halisi.
Baada ya ziara hiyo, Sitta alikataa kuzungumza lolote zaidi ya kusema: “Siruhusiwi kuongea chochote mpaka nikakapokabidhi ripoti bungeni.”
Kamati hiyo ilirejea Dodoma jana na kuwasili viwanja vya Bunge majira ya saa 10:45 jioni, baada ya kumaliza kazi ya kukutana na madaktari na serikali.
Awali kabla ya kamati hiyo kurejea, Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliwaambia wabunge waliokuwa wakihudhuria semina juu ya hali ya uchumi, kuwa wajumbe wa kamati hiyo walikuwa wamekodishiwa ndege kutoka Dar es Salaam ili watoe taarifa juu kwa Kamati ya Uongozi wa Bunge.
Alisema kamati hiyo itatoa taarifa hiyo kwenye kamati ya Bunge ya Uongozi wa Bunge pamoja na Waziri Mkuu, na kisha kujadiliana kabla ya kuwasilishwa bungeni.
WANAHARAKATI WAFUNGA BARABARA DAR
Wanaharakati jana waliamua kuingilia kati na kufunga barabara kwa lengo la kuishinikiza serikali ikutane na madaktari ili kuepusha vifo vinavyoendelea kutokea kutokana na wananchi kukosa huduma za matibabu.
Wanaharakati hao walifunga barabara jijini Dar es Salaam katika makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Ocean Road na kusababisha magari kushindwa kupita huku wakiwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali.
Maandamano hayo ambayo yaliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen-Kijo Bisimba na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya.
Baadhi ya mabango hayo yalisomeka “Rais Kikwete na Pinda tunataka afya bora, Rais Kikwete fukuza Waziri wa Afya, Naibu wake, Katibu Mkuu wake pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali kwa kuwa wameshindwa kufanya kazi.”
Mengine yalisema “Rais Kikwete hatibiwi Muhimbili, wabunge mmetusaliti sisi wananchi.” Wanaharakati hao waliondoka hapo baada ya saa 1:30 kwa amri ya Jeshi la Polisi.
Askari Polisi wenye sare na waliovalia kiraia wakiwa katika magari yenye namba za usajili T.313 AEN, PT 1848 na 778 AFG walizingira eneo hilo na kuwatangazia wanaharakati hao watawanyike na kufungua barabara ili kuruhusu magari kupita.
Waandamanaji hao walifika katika eneo hilo wakiwa kwenye magari yao na kuwakuta wenzao waliokuwa wametangulia na kuungana nao.
Bisimba alisema lengo lao lilikuwa ni kutaka kufikisha ujumbe kwa serikali kwamba wananchi wanakufa kwa kukosa huduma katika hospitali mbalimbali.
Alisema leo pia wanajipanga ili kufanya maandamano makubwa ambayo yatawashirikisha watu wengi zaidi.
Aidha, alisema wanaharakati wanalaani hatua ya Spika Makinda kuendelea kukataa suala la mgogoro wa madaktari kujadiwa kwa dharura bungeni huku akijua watu wanakufa.
Bisimba alisema wanajipanga ili kukusanya ushahidi wa watu waliokufa na kupata mateso kutokana na mgomo unaoendelea ili kuifikisha serikali mahakamani
BUNGE LAKWAMA KUJADILI
Sakata la mgomo wa madaktari jana limeibuka tena bungeni kwa mara ya sita, baada Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, kutoa hoja ya kutaka lijadiliwe kutokana na athari zake kuwa kubwa kwa jamii.
Alitoa hiyo hiyo siku moja baada ya Spika wa Bunge, Makinda kuzuia suala hilo kujadiliwa na wabunge akiwataka wavute subira hadi Kamati ya Bunge ya Ustawi wa Jamii itakapomaliza kazi yake na kutoa taarifa.
“Hii ni wiki ya pili sasa Wanzania wenzetu wanakufa mahospitalini kwa kukosa matibabu, kuna watu wanasema kujadili suala hili ni kuingilia mihimili mingine hii si sawa, hatuwezi kuendelea na kikao wakati Watanzania tunaowawakilisha hapa wanaendelea kufa…naomba kutoa hoja Bunge tujadili jambo hili kwa dharura,” alisema na hoja yake kuungwa mkono na wabunge wengine.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alikubaliana na Serukamba kuwa jambo hilo ni la dharura, hivyo linastahili kujadiliwa.
Baada ya kutoa maelezo hayo, Ndugai, aliielekeza Kamati ya Uongozi ya Bunge kukutana jana baada ya kipindi cha maswali na majibu ili kujadiliana na serikali namna ya kufanya kuhusiana na suala hilo.
MBATIA: VIGOGO WA WIZARA WAWAJIBISHWE
Mwenyeki wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushindwa kutatua mgomo wa madaktari na kulifikisha taifa katika hali ya hatari.
Akizungumza na waandishi habari jana jijini Dar es Salaam, Mbatia alisema kuna umuhimu wa watendaji hao kuwajibishwa au kujiwajibisha wenye kwa kuwa wamelifikisha taifa katika hali mbaya na matokeo yake kusababisha vifo.
“Chenji ya rada imerudi, basi hizo fedha zote zipelekwe kwa madaktari na sio kutoa kipaumbele katika mambo ambayo si ya muhimu,” alisema.
Mbatia alisema nchi haiwezi kuendelea kuongozwa huku watu wakiendelea kufa wakati serikali ina fedha.
Mbatia alisema ameshindwa kuelewa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Juduma za Jamii inafanya utafiti gani wakati jambo hilo linafahamika tangu awali na matokeo yake kupoteza muda huku wananchi wakiendelea kufa.
APPT MAENDELEO KWENDA KWA JK
Mwenyekiti wa Chama cha APPT Maendeleo, Peter Mziray, amesema chama chake kitakwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete kumweleza athari zinazoendelea kujitokeza na hatua anazopaswa kuzichukua kumaliza mgomo wa madktari unaoendeelea kuwaathili wananchi.
Alisema chama chake kimeamua kuchukua hatua hiyo baada ya ya kubaini kuwa wasaidizi wake (Rais) wameshindwa kulipatia ufumbuzi tatizo hilo kutokana na kulichukulia suala hilo kama la kisiasa.

Imeandikwa na Moshi Lusonzo, Richard Makore, Gwamaka Alipipi, Beatrice Shayo, Thobias Mwanakatwe, Dar; Abdallah Bawaziri, Sharon Sauwa, Dodoma; Emmanuel Lengwa, Mbeya; Charles Lyimo, Moshi na Juma Ng’oko, Mwanza.
CHANZO: NIPASHE
0 Maoni | Kuwa wa kwanza kutoa maoni

Nenhum comentário:

Postar um comentário